Luke 18:18-30

Mtawala Tajiri

(Mathayo 19:16-30; Marko 10:17-31)

18 a bMtawala mmoja akamuuliza Yesu, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”

19Yesu akamjibu, “Mbona unaniita mwema? Hakuna yeyote aliye mwema ila Mungu peke yake. 20 cUnazijua amri: ‘Usizini, usiue, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako.’ ”

21Akajibu, “Amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.”

22 dYesu aliposikia haya, akamwambia, “Bado kuna jambo moja ulilopungukiwa. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”

23Aliposikia jambo hili, alisikitika sana kwa maana alikuwa mtu mwenye mali nyingi. 24 eYesu akamtazama, akasema, “Tazama jinsi ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu! 25Hakika ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”

26Wale waliosikia haya wakauliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”

27 fYesu akajibu, “Yasiyowezekana kwa wanadamu yanawezekana kwa Mungu.”

28 gNdipo Petro akamjibu, “Tazama, tumeacha vyote tulivyokuwa navyo tukakufuata!”

29 hYesu akajibu, “Amin, nawaambia, hakuna hata mtu aliyeacha nyumba yake, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu 30 iambaye hatapewa mara nyingi zaidi ya hivyo katika maisha haya, na hatimaye kupata uzima wa milele ujao.”

Copyright information for SwhNEN